Avunja simanzi ya ujane na kuyakabili maisha
Mwananchi Kweli
3:49 AM
0
![]() |
| Mjane Magreth Levi Chiweza (45).akiuza vikapu alivyovifuma. |
Mjane Magreth Levi Chiweza (45), mkazi wa Njiro nje kidogo ya Manispaa ya Arusha, kama angeendelea kuomboleza kifo cha mumewe kwa muda mrefu bila ya kutumia akili ya kuanza kujipanga upya ili ayamudu maisha yake na watoto, sasa yake yangekuwa hayatabiriki.
Hakukubali kuwa kifo cha mumewe ndio mwisho wa maisha yake na familia yake.Mume wake alifariki mwaka 2010 na kumuachia watoto wanne kati yao wasichana ni wawili. Baada ya kifo cha mume wake maisha aliyumba kimaisha hata kujiona kama hana thamani duniani.
Mazingira hayo yalimfanya aukumbukie ujuzi wake alioupata mwaka 1985 alipojiunga na vikundi vya akna mama na kujifundisha kutengeneza vikapu, matenga ya kuhifadhia nguo,viti vya kupumzikia vya mianzi na vitu vinginevyo.
Magreth aliamua kuanza kutengeneza vikapu vya mapambo ya maua, vikapu kwa ajili ya mapambo ya maharusi na vingine vya kuhifadhia takataka.
"Nilijifunza ufundi huo kwa muda mfupi sana. Kilikuwa kipindi cha miezi miwili tu lakini ujuzi nilioupata ulikuwa muhimu sana. Nilijua kutengeneza vitu hivi kwa sababu tayari nilikuwa fundi wa kushona vitu mwenyewe na kusuka nywele za akina mama, hivyo kazi ya kujifundisha ufundi huo kwangu ilikuwa rahisi kama kumsukuma mlevi aliyekunywa pombe.
Nilijifunza huo kwa kuruhusiwa na mume wanegu kama vile alijua kuwa ipo siku hatakuwepo,"anasema huku akiangua kicheko.Kwa siku anasema kuwa, ana uwezo wa kutengeneza vikapu vitano na kuviingiza sokoni siku hiyo hiyo na kwamba siku ikiwa nzuri sana huuza vikapu vyote vitano.
Kapu moja huuza,kwa sh. 5,000 inategemeana na ukubwa wa kapu.Tenga la kuhifadhia nguo analiuza kati ya sh.15,000 hadi 20,000 na viti kila kimoja huuza kwa sh.25,000.Kwa upande wa vikapu vya kuhifadhia uchafu maarufu kwa jina la (Dustbin), huuza kwa sh.5,000 hadi 12,000 kutegemea na ukubwa wake Magreth anasema utengenezaji wa vitu hivyo sio mgumu sana kama mtu anadhamiria kujifundisha kwa bidii hata kama akiwa na kichwa kizito kushika mafundisho atafahamu tu kwa haraka.
Kimsingi tatizo kubwa katika uendeshaji wa biashara hiyo ni upatikanaji wa malighafi.
"Vifaa hivi vya kutengenezea vitu hivi vinapatikana kwa shida na huko porini kando kando ya mito au eneo la Ngaramtoni kwenye vijiji vya jamii ya Wamasai au eneo la Ilkiding'a na Kata ya Lemara,"anafafanua.
Anasema huko nako siyo kana mtu unaingia tu porini kuchukua hapana,wanalazimika kununua.Mwanzi mmoja huuziwa kwa sh. 100 .Shina zima la Mwanzi lenye mianzi mingi huuziwa kati ya sh. 20,000 na 50,000 kutegemeana na ukubwa wa shina.
Mwanzia anasema,ndio raslimali muhimu kwa ajili ya utengenezaji wa vitu vyake vingi.Vifaa vyake vingine anavipata nchini Kenya, kwenye mji wa Nairobi.Huko hufuata plastiki maalum za kutengenezea vikapu.
Wanauziwa bunda moja kwa sh. 40,000."Tukipata bunda moja tunatoa vikapu kama 28, na kapu moja tunauza kati ya 5,000 hadi 20,000 inategemeana na ukubwa ,"anasema Magreth.
Anasema anapenda kuwatia moyo wanawake wote wasikate tamaa au kufikiria kuwa kuanzisha biashara lazima uwe na mtaji mkubwa, hilo siyo kweli, kwa sababu yeye alianza na mtaji wa sh.100.Taratibu sasa mtaji wa vikapu vya mianzi umefika sh. 200,000 na vya plastiki sh. 300,000 na anaona kuwa anamudu maisha yake nafamilia kwa ujumla.
Hata hivyo, anasema wanapokwenda Nairobi hulazimika kuchukua bunda tano hadi kumi ili kupata rangi tofauti zitakazowawezesha kupata mchanganyiko mzuri kwa ajili ya kuvutia wateja.
Pamoja na upatikanaji huo, wanakumbana na changamoto kubwa ya kukosa eneo maalum la kuuzia bidhaa zao.Mazingira hayo huwalazimiha kujikuta wanapanga barabarani kwa kuvizia kwa sababu hufukuzwa na askari wa Manispaa kila mara kwa madai kuwa wanalichafua Jiji.
Changamoto nyingine anasema kuwa, kupata bidhaa ya plastiki ni ngumu sana mwezi wa Januari, kwa sababu kiwanda hufungwa kwa ajili ya kuhakiki mali na kufunga mahesabu ambayo wakati mwingine huchukua hata miezi miwili.
"Hali hii inatulazimu kununua bunda nyingi kwa ajili ya akiba wakati mwezi wa Desemba ili wakati huo ukifika tunandelea na shughuli zetu bila ya kukwama,"anasema.
Licha ya changamoto mbalimbali, anashukuru Mungu kuwa amefanikiwa kuhakikisha kuwa watoto wake wanapata elimu ya viwango mbalimbali, japo mtoto wake mkubwa alipochaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari alishindwa kumwendeleza kutokana na kukosa fedha sh. milioni moja wakati huo kwa sababu mtaji wake ulikuwa bado mdogo.
Kama hiyo haitoshi, Magreth amefanikiwa kuwafundisha ufundi huo wanawake wengine ili wachangamke na kuanza kutafuta fedha za kujikimu.Tayari amewafundisha akina mama wanne na wanaume watano.
Margeth anaiomba serikali iwaruhusu wajenge vibanda vya kudumu katika jiji la Arusha kwa ajili ya kuuzia bidhaa zao bila usumbufu kama ilivyo sasa wanafukuzwa kila mara na askari wa jiji ambao wakibahatika kuzikamata huzitaifisha na kwenda kuzifanya watakacho.
Miongoni mwa wanaume aliyemfundishwa kazi hiyo ni Athumani Mwedadi, anayebainisha kuwa amejikita zaidi katika uuzaji wa stuli anazotengeneza kwa mianzi ya porini.
Kabla ya kufundishwa kazi hiyo, alikuwa akijishughulisha na uoteshaji maua ya asili kwa ajili ya bustani, lakini yalikauka kwa sababu ya ukame mkali wa kiangazi na kuamua na kwenda kwa mama Chiweza kujifunza kazi za mikono.
"Namshukuru Mungu sana kwani sikosi riziki, japo tunapata usumbufu tu wa kufukuzwa na askari kila wakati, hili ni tatizo,
serikali ikitusaidia kutuondolea tatizo hili tukatulia sehemu moja kufanyabiashara hii hatutapata shida ya ajira na kuimudu familia,"anasema.
Anawashauri wanawake kwa waume kupenda kujishughulisha bila kujali kazi ya namna gani wanafanya kama tu ni halali ili mradi wanapata kipato.
Kwa upande wa wanaume wanaokataza wake zao kufanya kazi, waache kufanya hivyo sababu hawajui lini au nani atatangulia mbele ya haki na hivyo atakayebaki kama hana msingi mzuri ataadhirika sana.
CHANZO: NIPASHE

No comments