AZAM KUFURU KUBWA, Yachukua injini ya Yanga, Jangwani wajibu mapigo
Mwananchi Kweli
1:33 AM
0
Frank Domayo akisaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea timu ya Azam FC msimu ujao, msimu uliopita alikuwa akiichezea Yanga. Mpigapicha wetu
INJINI ndio roho ya gari aina yoyote ile, hakuna gari linaloweza kutembea wala kuwaka kama likitolewa injini. Azam FC imeng'oa injini ya kikosi cha Yanga.
Imemsainisha straika, Didier 'Mabao' Kavumbagu na Frank Domayo na sasa imetunisha misuli kwa nyota mwingine mmoja ambao kama wote waking'ooka tu, Yanga kitanuka.
Jana Jumatano mapema tu Azam ilianza mazungumzo na kiungo ambaye ni kama injini ya Yanga, Frank Domayo na kiraka Mbuyu Twite na ilipofika saa 1:30 usiku, ilifanikiwa kuinasa saini ya Domayo. Domayo ambaye yupo kwenye kambi ya Taifa Stars iliyopigwa Tukuyu, Mbeya alizungumza na viongozi hao wa Azam mapema na kumalizana kabla ya kumfuata kwenye kambi ya timu ya taifa na kumsainisha mkataba wa miaka miwili.
Domayo amemwaga wino kuichezea Azam FC kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kumaliza mkataba wake wa miaka miwili katika klabu yake Yanga aliyojiunga nayo miaka miwili iliyopita akitokea JKT Ruvu ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Twite kwa upande wake alikuwa na mazungumzo na Azam na Yanga jana Jumatano mchana na jioni na alikiri kwamba Azam wamemuahidi mambo mazuri. Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata ni kuwa Azam imepania kuwang'oa nyota hao, lakini Yanga na wenyewe wameweka mtego kwa kiungo makini wa Azam, Salum Aboubakary 'Sure Boy'. Hata hivyo, habari za kutoka ndani ya Azam zinabainisha kwamba Sure Boy ana mkataba wa miaka miwili hivyo itakuwa ngumu kwa Yanga kulipa kisasi kwa kumsajili kiungo huyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa Azam, Jemedari Said, alisema kwa mujibu wa ripoti ya Kocha Mkuu wa timu hiyo Mcamerooni, Joseph Omog, Azam inataka wachezaji sita kwa ajili ya kukiimarisha kikosi kiweze kucheza kiushindani Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
"Katika ripoti ya kocha tuliyoipokea, inaagiza kuwa tusajili kiungo wa kati mwenye kiwango kikubwa cha kucheza nafasi hiyo, mawinga wawili kushoto na kulia na kipa mwenye uzoefu wa kimataifa na hata beki wa pembeni hasa kulia.
"Yupo Manula (Aishi) mwenye uwezo mkubwa, lakini yeye hana uzoefu wa kucheza mechi za kimataifa, hivyo tunaendelea na usajili wetu wa kimya kimya kama tulivyofanya kwa Kavumbagu," alisema Jemedari ambaye aliwahi kuichezea Simba.
Kavumbagu aliiambia Mwanaspoti kuwa hatashangaa akisikia Twite amesaini Azam kwa vile Yanga bado hawaeleweki na amekuwa karibu na Twite anajua kila kinachoendelea.
Twite alipotafutwa kuzungumzia hilo, alisema: "Kiukweli kabisa, Azam nimepanga kukutana nao leo (jana Jumatano) jioni kwa ajili ya kusaini mkataba wa kuichezea timu hiyo.
"Yanga wameniita nimepanga kukutana nao kwa ajili ya mazungumzo ya kusaini mkataba mpya, majibu kamili nitayatoa mara baada ya kukutana nao wote."
Hata hivyo Twite na alipotafutwa baadaye jioni, akasema kwamba hawajafikia muafaka.
Naye Domayo kabla hajasaini Azam alisema: "Mimi nimebakiza mwezi mmoja na wiki kadhaa mkataba wangu umalizike, hivyo bado mchezaji halali wa Yanga." Kauli hiyo ya Domayo ilikuwa kabla hajakamilisha uhamisho wake wa kujiunga na mabingwa hao wapya wa Ligi Kuu Bara.
Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya kimataifa ya Yanga, Seif Ahmed 'Seif Magari' alisema: " Tunatambua kwamba Domayo mkataba wake upo ukingoni, tumeshafanya mazungumzo naye ya awali na mahitaji yake yote anayotaka yapo tayari, tunamsubiri ndugu yake mmoja aliyepo safarini arudi ili tumalizane.
"Kuhusu Twite tunaendelea naye na mazungumzo kwa ajili ya kumwongezea mkataba." Yanga wakawa wanaendelea kumsubiri ndugu yake Domayo arudi safarini, wenzao Azam wamefanya kweli na kumnasa kiungo huyo bora kabisa Tanzania.
Lakini, Mwanaspoti lilifahamu mapema kwamba msimamizi wa Domayo aliwazimia simu viongozi wa Yanga jana na siku nzima walikuwa wakihaha kumpata kabla ya jua kuzama na staa huyo wa Jangwani kutimkia Azam.
Yanga walikuwa kwenye msako wa kumnasa Domayo, jana Jumatano kuhakikisha wanazima jaribio la kiungo huyo kwenda Azam, kabla ya kuzidiwa ujanja kwa sababu tayari Azam walikuwa wameelekezwa kuonana na mjomba yake Domayo ambaye yupo jijini Dar es Salaam ambaye walimalizana naye juu ya usajili wa mchezaji huyo.
"Tulisikia Azam wanataka kumalizana naye leo (jana Jumatano) mchana, tuliona haitawezekana Azam watuchukulie injini yetu, tumehangaika sana kuhakikisha anabaki Yanga lakini cha ajabu Domayo alituelekeza kuwa tumalizane na mjomba yake aliyepo Dar es Salaam.
"Tumefuatilia na kugundua kuwa mjomba wake huyo alikuwa amemalizana na Azam ambapo tumeambiwa waliahidi kumpa Sh50 milioni na sisi tulikuwa na Sh40 milioni tulizotaka kumwingizia kwenye akaunti yake ya benki, kuna mchezaji wetu ambaye tunamtumia ili kumshawishi abaki kwetu," kilisema chanzo hicho.
Usajili bado haujaanza rasmi lakini Azam imechafua hewa na kuzistua timu kongwe baada ya kuanza usajili kwa fujo.
Viongozi wakamatwa
Taarifa zilizoifikia Mwanaspoti, ilipotimu saa 1:30 usiku Domayo alisaini kuichezea Azam, ambapo kazi hiyo ilifanyikwa na viongozi wanne wa Azam katika moja ya vibanda kwenye hoteli ya Landamark ambayo ndiyo kikosi cha Taifa Stars kimeweka kambi katika eneo la Tukuyu mjini.
"Tumekamilisha zoezi la kumsainisha Domayo hivi sasa baada ya awali kumalizana na ndugu yake hapa jijini Dar es Salaam ambaye ndiye aliyepokea fedha za usajili, lakini tukalazimika kutuma vijana wetu Mbeya alipo mchezaji mwenyewe ili asaini fomu za usajili na baadhi ya makaratasi hayo ya usajili yakamatwa, kama unavyojua huyu kijana yupo katika kambi ya timu ya taifa sasa," alisema mmoja wa mabosi wa Azam.
Kutokana na muda mfupi baada ya kukamilisha zoezi hilo, viongozi hao wa Azam akiwemo na mjomba wake ambaye ndye meneja wa mchezaji huyo walikamatwa kwa kuingia katika eneo la kambi hiyo bila kibali cha wahusika ambapo inaelezwa kuwa mpaka jana usiku walikuwa wameshikiliwa na polisi kwa kosa hilo la kuvunja kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
"Tumefanikiwa kuwakamata watu wawili mmoja tumeambiwa ni kiongozi wa Azam mwingine ni ndugu wa huyu mchezaji ambaye muda mfupi baada ya kukamatwa alikuwa akitutolea lugha chafu ambazo tulilazimika kumkamata na sasa wanashikiliwa chini ya ulinzi," alisema meneja wa Taifa Stars, Clement Boniface alipozungumza na Mwanaspoti jana usiku.
Mwanaspot

No comments